ZITTO KABWE AHOJI VIWANGO VYA UBORA WA NDEGE INAYONUNULIWA NA SERIKALI AINA YA DREAMLINER, ADAI ZILIKATALIWA NA MASHIRIKA MENGINE


Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amehoji viwango vya ndege inayonunuliwa na Serikali aina ya Dreamliner akisema ndege hizo zilikataliwa na mashirika mengine ya dunia kutokana na ubora wake.
Hiyo ni moja kati ya ndege ambazo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imepanga kuzinunua katika mkakati wake wa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Tayari imeshanunua mbili aina ya Bombardier.

Zitto alisema hayo katika mchango wake wa maandishi kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano juzi usiku. Mjadala huo wa siku tatu utaendelea Jumanne ijayo ambapo Waziri Makame Mbarawa atajibu hoja za wabunge.

“Ndege hizi zinaitwa ‘Terrible Teens Dreamliners’ ambazo zilikuwa 12 na zilikosa soko kwa sababu ni nzito na hazina viwango,” alisema.

Alisema pia Ethiopia imenunua ndege hizo lakini kwa punguzo kubwa la bei kwa sababu hazikuwa na soko.

“Wajibu wangu kama mbunge ni kuisimamia Serikali na kuhakikisha fedha za Watanzania zinatumika kwa uwazi na kwa umakini. Hivyo naomba maelezo ya Serikali kuhusu suala hili ili Watanzania wajue kama fedha zao zinatumika vizuri,”alisema.

Alisema mwaka jana, Serikali ilitenga Sh500 bilioni kununua ndege na mwaka huu pia kiasi kama hicho na tayari imelipa asilimia 30 ya dola za Marekani 224 milioni kununua Dreamliner.

Zitto alisema kwa miaka miwili, zimetumika Sh1 trilioni ambazo ni alisema ni uamuzi mgumu wakati hakuna chakula katika Ghala la Taifa na watoto wanakosa mikopo ya elimu ya juu kwa sababu tunanunua ndege.

“Bajeti ya mbolea ya ruzuku kwa wakulima wetu imepungua kutoka Sh78 bilioni mpaka Sh10 bilioni kwa sababu tunanunua ndege, fedha ya vifaa tiba na dawa hospitalini ni ndogo kwa sababu tunanunua ndege. Ni maamuzi. Kupanga ni kuchagua,” alisema.



Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0753 336 000

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.