WATUMISHI WENYE VYETI FEKI WAANZA KUJIONDOA

Rais Magufuli wakati akipokea ripoti ya ukaguzi wa vyeti vya watumishi wa umma mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma, aliagiza watumishi ambao wamebainika kuwa na vyeti feki wajiondoe katika kazi kabla ya Mei 15, mwaka huu, vinginevyo baada ya hapo watafikishwa mahakamani.

Kutokana na agizo hilo, Nipashe imefanya uchunguzi kutoka katika baadhi ya mikoa na kubaini baadhi ya watumishi wameanza kuondoka ikiwa hatua ya kutii agizo la Rais Rais Magufuli.

Mikoa ambayo watumishi wameanza kujiondoa ni Mbeya, Manyara, Lindi na Tanga na Kilimanjaro.

Katika taarifa ya uhakiki wa vyeti hivyo, ilibainika kuwa watumishi 9,932 walitumia vyeti vya kughushi kupata ajira na Rais John Magufuli alisema watu hao ni sawa na wezi na majambazi, hivyo wajiondoe kufikia Mei 15, mwaka huu, kabla hawajafikishwa mahakamani.

Aidha, Rais Magufuli aliagiza pia watumishi hao wenye vyeti feki wasilipwe mishahara na nafasi zao za kazi zitangazwe ili wenye sifa waombe na kuajiriwa ili wazizibe.

Alisema pamoja na kuzuia mishahara yao, Wizara ya Fedha na Mipango inatakiwa kuwaondoa kwenye mfumo wa mishahara watumishi hao ambao hawana sifa ya kufanya kazi.


Katika ripoti hiyo iliyokabidhiwa kwa Rais na Waziri Kairuki, ilibainika vilevile kuwa watumishi wa umma 1,538 wamekuwa wakitumia vyeti vinavyofanana taarifa huku wengine 11,596 wakiwa na vyeti visivyokamilika kwa kuwa na vya kitaaluma bila ya kuwa na vyeti vya kidato cha nne na cha sita.


Hata hivyo, alisema watumishi hao walioingiliana majina wamepewa hadi Mei 15, mwaka huu, wawe wamejitokeza au wale wanaomini ‘wameiba’ majina ya wengine, kuachia ngazi mara moja.


Watumishi hao baada ya kufanyiwa uhakiki vyeti vyao, waligundulika kufanana majina, vyeti na shule, hali iliyomfanya Rais Magufuli kuzuia kulipwa mishahara yao hadi hapo Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma) itakapotatua tatizo lao.


Miongoni mwa watumishi hao waliogundulika wanatumia vyeti vya kughushi, baadhi yao walikuwa watumishi wanaolipwa mishahara mikubwa na kuishi maisha ya kifahari, lakini kwa uamuzi huo wa serikali wengi wao njaa itaanza kuwatembelea.


Hali hiyo inatokana na mirija yote waliyokuwa nayo ya kupata fedha, kuzibwa kuanzia mishahara hadi ‘michongo’ mingine ya kazini.


Baadhi ya watumishi hao, walikuwa wakisomesha watoto nje ya nchi au shule za gharama nchini, hali itakayosababisha familia nyingi kuyumba kwa kukosa fungu la fedha.


MBEYA
Katika mkoa wa Mbeya baadhi ya viongozi waandamizi wa mkoa nusura washindwe kuhudhuria katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) juzi baada ya madereva wao kuingia ‘mitini’.


Taarifa zilieleza kuwa madereva hao ni miongoni mwa watumishi waliokumbwa na sakata la vyeti feki.


Baadhi ya madereva wanaosemekana kuingia mitini ni pamoja na aliyekuwa akimwendesha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya na Katibu Tawala wa Mkoa huo.


Katibu Tawala wa mkoa huo, Miriam Mtunguja, akizungumza na Nipashe alikiri baadhi ya madereva hao kuondoka na kwamba licha ya kufanya hivyo, hajawaathirika chochote kwa sababu walibadilisha madereva wengine.


“Ni kweli kuna baadhi ya madereva wameondoka na si wa viongozi hao tu, lakini nina taarifa kuwa watu wengi wameondoka, lakini kwa sasa bado nafuatilia zaidi kuhakiki,” alisema.


MANYARA
Kutoka Manyara, Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Joel Bendera, alisema amepata taarifa kwamba baadhi ya madaktari na wahudumu wa sekta ya afya wameshaondoka japokuwa hakutaja idadi yao.


“Ni kweli baadhi ya watumishi wanaodaiwa kufoji vyeti wameanza kuondoka na nimepata taarifa za kuondoka madaktari na wahudumu wengine wa sekta ya afya,” alisema.


LINDI
Katika mkoa wa Lindi nako, baadhi ya watumishi ambao wanadaiwa kughushi vyeti wameanza kuondoka huku baadhi ya huduma zikianza kudorora.


Kwa mfano katika zahanati za Mkanga na Sudi, inasemekana baadhi ya madaktari na wahudumu wameshaondoka, hivyo kusababisha baadhi ya huduma kusuasua.


Habari zaidi zinaeleza kuwa watumishi 236 wa serikali mkoani humo walioorodheshwa kuwa na vyeti feki, wengi hawakuonekana kazini kwa siku ya jana.
Alisema watumishi wengi ni wale wanaotoka kalmashauri za wilaya za Nachingwea na Kilwa.


Mkuu wa Mkoa huo, Godfrey Zambi alisema wilaya ya Nachingwea inaongoza kwa kuwa na watumishi (72), ikifuatiwa na Kilwa (53), Ruangwa (45), Lindi (25), Ofisi ya Katibu Tawala (RAS) (23), Manispaa ya Lindi (11) na Liwale 17.


Zambi amesema katika idadi hiyo, idara za afya na elimu ndizo zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watumishi waliobainika kuwa na aina hiyo ya vyeti.


TANGA
Katika Wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga, zaidi ya watumishi 70 ambao wamepatikana na tuhuma ya kughushi vyeti wameanza kuzikimbia maeneo ya kazi.


Baadhi ya watumishi hao, wakiwamo wale wanaofanya kazi ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, jana walionekana wakifungasha virago baada ya kuona majina yao katika vyombo vya habari.


Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Waziri Kombo alisema watumishi hao wameshafungasha virago baada ya majina yao kutangazwa katika magazeti.


Hata hivyo, Kondo alisema baadhi ya watumishi wamelalamikia uhakiki huo kwa kudai kuwa wana vyeti halisi na si bandia kama ilivyoelezwa na kwamba baadhi wamegoma kuondoka kama walivyoamuriwa.


KILIMANJARO
Katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, watumishi wasiyo na vyeti waliobainika ni 60 ambao tangu kutangazwa kwa majina yao wamekacha kwenda kazini.


Chanzo kimoja kutoka Halmashauri ya Manispaa hiyo, kililieleza Nipashe kuwa, watumishi hao waliacha kwenda kazini bila taarifa maalum tangu majina yao yalipotangazwa.


Kilieleza zaidi kuwa, kati ya watumishi hao 60, wanne kati yao walipeleka malalamiko kuwa wana vyeti halali licha ya kutajwa katika orodha hiyo.


“Watumishi wote wameacha kuja kazini tangu Rais Magufuli, alipopokea majina yao isipokuwa wanne walikuja na vyeti vyao halali wakilalamikia kuingizwa kwenye orodha hiyo,” kilieleza chanzo hicho.


Kadhalika kilieleza kuwa, watumishi hao wamepanga kwenda mkoani Dodoma kwa ajili ya kupeleka malalamiko na ushahidi wa vyeti vyao ili kupatiwa ufumbuzi.


Uchunguzi wa Nipashe kwenye idara mbalimbali umebaini kuwa watumishi wengi waliotajwa kuwa na vyeti feki wamezikimbia ofisi kwa kujua kuwa mwezi huu hawataingiziwa mishahara.




Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Mary Geofrey (Dar), Stephen William (Tanga) na Ramadhan Hamdan (Lindi).

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0753 336 000

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.