ATIWA MBARONI KWA MAUAJI YA TEMBO

POLISI wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, wanawashikilia wakazi wanane wa kijiji cha Wenje kwa tuhuma za kujihusisha na mauaji ya tembo wawili yaliyotokea kijijini hapo Aprili 18, mwaka huu.
Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa, baada wananchi hao kutekeleza mauaji hayo , waling’oa meno mawili kutoka katika tembo mmoja na kutokemea nayo.

Tembo hao walikutwa wakiwa pembezoni mwa mashamba ya wananchi huku wakiwa wamebaki mifupa mitupu baada ya nyama yake kusadikiwa kuliwa na baadhi ya wakazi wa maeneo hayo.

Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Wenje, Chamba Maganga, alisema baada ya tembo hao kuripotiwa kuwa wamevamia mashamba ya wakulima, kwa kushirikiana na wasamaria wema walitoa taarifa kwa viongozi wa Idara ya Wanyamapori wilayani hapa kwa ajili ya kwenda kuwafukuza.

Alisema wakati akiwa katika harakati hizo, alipokea taarifa kuwa wananchi hao waliodai kuvaiwa na tembo hao wamekwishawaua tembo wawili, jambo ambalo limefanya aende katika eneo la tukio na kuwakurupusha majangiri hao.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Ujangili, Henry Mwaibambe, aliwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Juma Ally (36), Mwinyi Mng’ol e(24), Salum Asiki (46) na Kalengo Mkanda (45).

Kwa mujibu wa Mwaibambe, watuhumiwa wengine ni Fadhili Mang’ambila (43), Abdallah Sahibu (37), Ahmad Yasini (30) na Rashid Ausi (46) smbao watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria wakati wowote.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Kuzuia Ujangili Tanzania, Robert Mande, ambaye pia alishiriki katika oparesheni hiyo, alisema kitendo cha majangili hao kuua tembo, kumeipunguzia nchi fedha za kigeni ambazo zingetokana na watalii kuja kuwaona na kupiga picha na wanyama hao ambao ni urithi wa taifa.

Mande alisema watu wengi wamekuwa wanashindwa kuelewa maana na thamani ambayo imekuwa ikielezwa na wataalamu kwamba tembo mmoja thamani yake ni dola za Marekani 150 haihusianai na thamani yao.

Naye Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera, alisema serikali haitawafumbia macho wale wote ambao wamekuwa wanajihusisha na matukio ya ujangili.
Homera pia alisema kuanzia sasa watuhumiwa wa ujangili watasakwa kwa udi na uvumba na kuhakikisha wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0753 336 000

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.